Waziri Mkuu ahitimisha ziara yake na Tsh. Bilioni 1.5 za Hospitali
Serikali imepanga kutoa Tsh. Billioni 1.5 katika mpango wa awamu ya pili za Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza ili kuboresha utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wengi kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-toure.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa ahadi hiyo ya Serikali wakati akizungumza na Wananchi wa Koromije Wilayani Misungwi katika ziara aliyoifanya jana kwa lengo la kufuatilia utekelezaji na ufunguzi rasmi wa mradi wa ujenzi na ukarabati mkubwa wa Kituo cha Afya Koromije uliogharimu fedha zaidi ya Tsh. Milioni 500 zilizotolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambapo Majengo matano yamekamilika ikwemo jengo la Maabara, Upasuaji, Wodi ya Wazazi,Nyumba ya Mganga na jengo la kuhifadhia maiti,sambamba na kujenga majengo hayo matano Halmashauri imefanikiwa kujenga na kukamilisha jengo la ziada la X-ray kutokana na fedha zilizotolewa.
Waziri Mkuu wa Tanzania alifurahishwa sana na kuwapongeza Kamati ya ujenzi,Viongozi wa Wilaya, Kata na Kijiji na wananchi wote kwa kushiriki na kusimamia kikamilifu ujenzi na ukarabati huo uliofanywa kwa kiwango na ubora, na kuwaomba wananchi kuiamini Serikali ya awamu ya tano ambayo imeweka mkakati madhubuti wa kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya nchini kote,
"Tayari Vituo vya Afya 340 vimejengwa na kukarabatiwa nchi nzima na Serikali inaendelea kutoa fedha zingine kwa awamu ya pili za ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya na fedha za ununuzi wa madawa na vifaa tiba kwa malengo mapana ya kuboresha huduma za upasuaji mdogo na mkubwa," alisema Waziri Mkuu.
Amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Misungwi kwa kushirikiana na Vijiji kuhamasisha na kuanzisha pamoja na kusimamia ujenzi wa Zahanati katika kila Kijiji ambao ni ujenzi wa angalau vyumba vitano tu muhimu kwa ajili ya utoaji wa huduma za Afya za awali kwa Magonjwa ya kawaida, pamoja na kuongeza majengo mengine ya Wodi ya Wanaume na Wodi ya watu wenye magonjwa mchanganyiko katika Kituo cha Afya cha Koromije ili kuwezesha wananchi wengi kupata huduma bora za Afya kwa ukaribu na haraka zaidi.







0 comments:
Post a Comment