Wabunge Manyara wahofia maswali magumu Bungeni bila majibu
Na, John Walter- Manyara
Wabunge wa mkoa wa Manyara wameonyesha wasiwasi wa kukutana na maswali magumu katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao wa 2020 kutokana na kutotekelezwa kwa ahadi za Rais alizozitoa katika kipindi cha Kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015.
Hayo yamesemwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Manyara (RCC) kilichohudhuriwa na wabunge wote wa mkoa huo, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wataalam kutoka Sekretarieti ya mkoa na ikiongozwa na mwenyekiti wake mkuu wa mkoa Alexander Mnyeti akisaidiana na Katibu Tawala wa mkoa.
Ahadi zilizolalamikiwa kutotekelezwa, nyingi zilihusu ujenzi wa barabara, ambapo mbunge wa jimbo la Mbulu mjini Zakaria Isaay alieleza kuwa ahadi ya Rais katika Jimbo lake ni Km.5 kwenye barabara ya mlima Magara na badala yake ujenzi uliotekelezwa ni wa Mita 300 na kutupia lawama Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), kwa madai ya kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mbunge mwingine aliyeonyesha wasiwasi wa kukutana na maswali magumu ni mbunge wa Jimbo la Kiteto Emanuel Papian aliyelalamika kwa kutotekelezwa kikamilifu ahadi za Rais hasa kwa upande wa ujenzi wa barabara.
Naye mbunge wa Jimbo la Hanang Mary Nagu alisema TARURA wamepewa majukumu ya kukarabati barabara,ila kinachoonekana ni kwamba hawapewi bajeti ya kutosha kutekeleza kazi zilizopo pamoja na zile za ahadi za Rais,”Tusiwalaumu TARURA kushindwa kutekeleza ahadi za Rais bila kujua bajeti wanayopewa.
TANROAD wana jumla ya Km.1656 wanapokea asilimia 70 na TARURA wana jumla ya Km.5743 wanapata asilimia 30 ya fedha za mfuko wa barabara za mkoa.
Mkoa wa Manyara katika mpango wake wa bajeti ya mwaka 2019/2020 ina mpango wa kuwekeza katika kilimo hasa uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mazao ya kilimo.
Mambo Mengine ni kuongeza mapato ya ndani,kuondoa upungufu wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na maabara pamoja na kutengwa fedha kwa ajili ya kuendeleza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati.







0 comments:
Post a Comment