Serikali yawataka wananchi kushiriki katika miradi ya maendeleo
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Afya kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kutoa ushirikikiano katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo ili kuleta maendeleo na kupunguza changamoto za afya nchini.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo katika kijiji cha Mlowa Barabarani wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikiwa katika kuleta maendeleo bila kuwepo ushirikiano kutoka kwa wananchi wake hivyo ni vyema wananchi wakashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Amesema Serikali imejenga miundombinu ya afya nchini ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma za afya zinaboreka kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali za Mikoa ili kupunguza changamoto katika sekta ya afya.
Akiendelea kufafanua amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kusimamia miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ili zijengwe kwa ubora kulingana na fedha zilizotolewa na Serikali.
“Wananchi hakikisheni mnasimamia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino kwa umakini mkubwa kwa kuangalia gharama zinazotumika zinaenda sambamba na majengo yanayojengwa kwa kuwa Hospitali hizi ni mali ya wananchi” Amesisitiza Gwajima
Akifafanua kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya amesema Serikali imejenga miudombinu ya afya nchini lakini bado changamoto kubwa ni watendaji waliopo katika vituo hivyo kutotimiza majukumu yao kwa uadilifu katika kutoa huduma bora kwa jamii hali ambayo inasababisha wananchi wengi kutokufika katika vituo hivyo.







0 comments:
Post a Comment