Friday, 20 May 2016

Wanne wasimamishwa kazi Mpwapwa.


BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, limeridhia kuwasimamisha kazi watumishi wanane wa halmashauri hiyo kwa kipindi tofauti kupisha uchunguzi wa awali, baada ya watumishi hao kutuhumiwa kufanya makosa ya kinidhamu, kiutumishi huku mwingine akituhumiwa kughushi cheti cha kidato cha nne.

Akisoma majina ya watumishi waliosimamishwa kazi, Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Dorica Dorio alisema miongoni mwao ni Kaimu Mhandisi Idara ya Ujenzi, Yason Magombana anayetuhumiwa kujenga chini ya kiwango baadhi ya miradi, ikiwemo zahanati ya kijiji cha Singonari Kata ya Rudi, daraja la kijiji cha Bumira, zahanati ya kijiji cha Chamanda na Kituo cha Mawasiliano ya Taaluma Kibakwe.

Mwingine ni Samweli Koyi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha manunuzi ambaye amesimamishwa kwa siku 14 kupisha uchunguzi kwa tuhuma za kutoa taarifa yenye mapungufu mengi na ikiwa hati ya agizo (LPO) moja yenye tarehe moja kuwa na malipo tofauti na vitu kununuliwa kwa bei kubwa tofauti na uhalisia wa bidhaa inavyouzwa sokoni.

Aidha, alisema watumishi wengine waliosimamishwa ni Kaimu Ofisa Mifugo Msaidizi, Peter Njau, Vincent Meshack, na Henry Msukulu walisimamishwa kazi kwa siku tisini kwa tuhuma za kutumia fedha bila kufuata utaratibu, na kukiuka taratibu za manunuzi ya kukusanyia fedha na taratibu za kutoa vitabu hivyo.

Alisema mtumishi mwingine aliyesimamishwa kazi ni Ibrahimu Butta aliyetuhumiwa kughushi cheti cha kidato cha nne na kujipatia ajira kinyume cha sheria.

Watumishi wengine walio simamishwa kazi ni Paul Ngwembele, Elly Mwakyusa kwa kutokuwapo kazini kwa muda bila taarifa kinyume na kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 kanuni na 57 (1).

Pia baraza hilo limeridhia kupitisha jina la Benedict Ngailo kuwa Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani na Gabriel Mnyawami kuwa Mwenyekiti wa bodi ya ajira katika halmashauri hiyo.

0 comments:

Post a Comment