Rais Dk John Pombe Magufuli.
BAADHI ya vigogo ambao ni watumishi wa muda mrefu serikalini, wameamua kuwarudisha nyumbani watoto wao waliokuwa wakisoma nje, ili waendelee na masomo kutokana na staili ya kubana matumizi inayofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Kwa mujibu wa chanzo kilicho serikalini,
mianya mingi iliyokuwa ikitumiwa na vigogo hao kupata fedha, kama vile
semina, vikao, kongamano na safari kufutwa na hivyo kuwafanya waishi kwa
vipato vyao halali.
“Zamani kulikuwa na vyanzo vingi vya
hela zaidi ya mshahara, mtu angeweza kupiga simu moja au mbili, tayari
ameingiza fedha, lakini hivi sasa kila sehemu imebana, watu
wanawarudisha vijana wao nyumbani kwa sababu siyo rahisi kumudu gharama
za masomo kwa mishahara,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilidai kuwa maofisa wa
serikali hivi sasa wamekuwa waoga hata kuchukua pesa halali kwa hofu ya
kutumbuliwa, kwani hakuna dalili kama spidi ya kubana matumizi
inayochukuliwa na Rais Dk John Pombe Magufuli itapungua.
Ofisa mmoja wa Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi ambaye alikataa kutumiwa kwa jina lake kwa vile
siyo msemaji, alisema watoto wanaosoma nje hurejea nyumbani mara kwa
mara, hivyo ni vigumu kujua kama ni sababu ya ukata wa wazazi wao au
kuna sababu zingine.
“Sehemu nzuri ambako unaweza kupata data
ni kutembea katika mashule, hasa binafsi ambako watoto wengi wa
watumishi mabosi wa serikali wanasoma, lakini hili la kurejea nchini ni
la kweli,” alisema ofisa huyo.
Tangu kuingia madarakani kwa serikali ya
awamu ya tano, kumekuwa na shinikizo la kubana matumizi ya fedha za
serikali, ikiwemo kukataza vikao vya kulipana posho visivyo na tija,
safari holela za ndani na nje pamoja na kuondolewa kwa sherehe zisizo na
tija.
0 comments:
Post a Comment