Friday, 20 May 2016

MISIMU 17 VPL, MTIBWA SUGAR ITAENDELEA KUMPA NAFASI SHAABAN NDITTI.

Nditi-Gervinho

Shaaban nditti anamaliza msimu wake wa 17 mfululizo katika ligi kuu Tanzania bara na mchezaji huyo wa zamani wa Taifa Stars bado ana nguvu, maarifa, mbinu, na uwezo wa kupambana bila kuchoka na wachezaji vijana.

Wakati wengi ‘wameingia na kutoka’ katika ligi kuu bara, Nditti amedumu tangu mwaka 1999 alikoanza soka lake akiwa na timu ya Singida United ya Singida. Alisajiliwa na Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza mara baada ya Mtibwa kutwaa ubingwa wao wa pili mfululizo wa VPL mwishoni mwa 2000.

Nditti aliondoka Mtibwa na kusajiliwa na Simba mwishoni mwa mwaka 2003 lakini alishindwa kutulia klabuni hapo na baada ya kumalizika kwa msimu wa 2004 akaamua kurejea Mtibwa ambako amedumu kwa miaka 12 mfululizo bila kuhama huku akitumia misimu miwili tu kati ya 17 kucheza nje ya timu hiyo ya Turiani, Morogoro.

Akiwa mshindi wa taji la ligi kuu mwaka 2004 akiwa na Simba, Nditti ameichezea timu ya Taifa kwa miaka zaidi ya kumi na kila kocha wa kigeni kuanzia, Mbrazil, Marcio Maximo (2006 hadi 2010,) Wadenish JAN na KIM Poulsen wote walipendezwa na nidhamu ya Nditti, mchezo wake wa uhakika akiwa katikati ya uwanja.


Liuzio ni mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Mtibwa kisha ile ya wa kubwa alicheza na Nditti kwa misimu miwili klabuni Mtibwa. “Nidhamu yake nje na ndani ya uwanja ndiyo silaha yake kubwa, nilimpokea kwa mara ya kwanza akiwa kijana mdogo pale Singida. Mungu amsimamie ‘my young brother’ Nditti.” ni maneno ya mlinzi wa zamani wa Yanga SC, Mzee Abdallah.
Nilimtafuta msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru na kutaka kufahamu kama wataendelea kuwa Nditti msimu ujao.

“Amekuwa kiongozi mzuri kwa wachezaji ndani na hata nje ya uwanja. Amekuwa hapa kwa miaka zaidi ya 14, hapa ni nyumbani kwake na sisi kama Mtibwa tunafarijika kumuona akicheza katika kiwango cha juu kila msimu. Bado tunahitaji huduma na ya kapteni wetu Nditti lakini kwa sasa siwezi kusema zaidi, ila Nditti atabaki Mtibwa na tutakuwa nae msimu ujao”, anasema Kifaru.

0 comments:

Post a Comment