Friday, 20 May 2016

Ofisa TRA, TPA watuhumiwa kuficha mamia ya televisheni.


MAOFISA wawili, mmoja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na mwingine wa Mamlaka ya Bandari (TPA) wilayani hapa, wanatuhumiwa kuhusika na tukio la kuficha televisheni zenye muundo bapa (flat screens) 288. Walitajwa kuwa ni Hadji Nyagawa wa TRA, Idara ya Forodha na Hamis Yusufu wa TPA.

Televisheni hizo zilifichwa juzi kwenye vyoo tayari kusafirishwa kwa kutoroshwa kupitia bandari ya Kilwa Masoko, wilayani humu. Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Godfrey Zambi, Meneja wa TRA Mkoa, Emmanuel Makwaba na maofisa wengine walitembelea juzi bandari hiyo hadi vyooni zilikofichwa televisheni hizo.

Ilielezwa kuwa zilikuwa katika choo namba 3 na 4 na sasa zimepelekwa katika kituo cha Polisi cha Wilaya. Zambi, baada ya kujiridhisha na tukio hilo aliamuru Polisi mkoa kuwakamata maofisa hao Nyagawa na Yusufu na kuwashikilia kwa uchunguzi zaidi kutokana na tuhuma hizo.

Aliyetoa taarifa ya tukio hilo kwa Mkuu wa Mkoa huo ni msamaria mwema. Imeelezwa kuwa, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kufichwa bidhaa huku nyingine zikisafirishwa kwa magendo na kukwepa kulipa kodi. Hivi karibuni ilikamatwa sukari kutoka India, Brazil na mafuta ya kula kutoka Malaysia

0 comments:

Post a Comment