Tuesday, 26 March 2019

Wenye magari ya Kemikali za kulipua watakiwa kupata vibali

Wenye magari ya Kemikali za kulipua watakiwa kupata vibali


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema magari yanayobeba kemikali za kulipuka yanatakiwa kupata kibali cha Mkemia Mkuu wa Serikali na si kibali kutoka kwa Wakala wa Barabara (Tanroads).

Kamwelwe alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo sekta ya ujenzi. Alisema ameona atoe ufafanuzi huo kutokana na mkanganyiko uliopo wa utoaji wa vibali.

Waziri huyo alisema kuna sheria wanazotekeleza lakini kuna mkanganyiko juu ya gari linalobeba kemikali za kulipuka zinapewa kibali na mkemia mkuu wa serikali na si Tanroads na magari hayo hayawezi kupita kwenye mizani kama huna kibali cha mkemia. “Pia nataka wahusika kwenye wizara yangu watoe ufafanuzi magari yanayobeba milipuko yanapimwa au hayapimwi kwenye mizani,"alisema.

Pia alisema kuna sheria ya uzito wa magari na sheria hizo watazipitia na kutoa maelekezo. Waziri huyo alisema ripoti ya miradi ya wizara hiyo iliyopitiwa na kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu imeonekana kuwa na upungufu mwingi. Kamati ya Bunge ya miundombinu ilipitia mradi wa ujenzi wa viwanja vya ndege jijini Dodoma, Dar es Salaam na mradi wa barbara mkoani Mtwara.

Alisema amepewa taarifa na kamati hiyo kuwa ripoti hiyo ni mbaya haina ufanisi wowote kulingana na miradi hiyo. Alitoa siku moja ili ripoti hizi ziandikwe upya kutokana na kuhofia kushambuliwa na wabunge kutokana na ripoti hiyo. Hata hivyo, alisema wanatakiwa kwenda kukesha ili kuhakikisha wanabadilisha ripoti hizo. "Naomba leo msilale hakikisheni mnamaliza hiyo ripoti," alisema Kamwelwe.

Alisema hakuna kilichofanyika kutokana na kwamba kamati hiyo imeiponda sana hiyo ripoti. Pamoja na hayo alilitaka Baraza hilo kutoa matokeo chanya kwani dhana ya Baraza mahali pa kazi ni ushirikishwaji. Alisema madhumuni ya baraza ni kutoa fursa kwa watumishi juu ya masuala yanayohusu maslahi yao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo sekta ya ujenzi, Elius Mwakalinga alitaka kila mshiriki alitendee haki Baraza hilo kwa kutoa mchango ambao utakuwa na tija na wenye lengo la manufaa. Pia alisema wamejipanga kuwajengea uwezo wataalamu ili wawe mahiri. Pia kuboresha mifumo ya magari ili kuepuka foleni kwenye vituo vya mizani.

0 comments:

Post a Comment