Wachimbaji wadogo wafundwa kusajili mikataba ya uchimbaji madini
Wachimbaji wa madini ya tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, wametakiwa kusajili mikataba ya uchimbaji wanaoingia na raia wa nje kwenye Wizara ya Madini.
Ofisa Madini Mkazi wa Simanjiro, Daudi Ntalima, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wachimbaji wa madini ya tanzanite mji mdogo wa Mirerani.
Ntalima alisema mikataba yote wanayoingia na wageni inapaswa kusajiliwa wizarani na maelezo yatatolewa ofisini kwao.
Aliongeza kuwa wamiliki wa migodi wanapaswa kupewa utaratibu wa kusajili mikataba hiyo na serikali ikague kubaini namna watakavyonufaika na uwekezaji huo wa wageni.
"Mnapaswa kuishirikisha Wizara ya Madini ili itambue mikataba hiyo na wageni na pia baadaye yasije yakatokea mambo ya kudhulumiana mkashindwa kupata msaada," alisema Ntalima.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Justine Nyari, alisema suala hilo watalifikisha kwa wachimbaji wote ili kuhakikisha mikataba yote ya uwekezaji inajulikana na kufikishwa ofisi ya madini.
Alisema wataendelea kushirikiana na serikali katika uchimbaji madini kwa kuwa wizara ndiyo walezi wa wachimbaji wote nchini hivyo watahakikisha hilo linatekelezwa.







0 comments:
Post a Comment