Sheria mpya ya udhibiti uzito kuanza rasmi
Serikali imesema kuwa sheria mpya ya mizani inayowataka madereva na wamiliki kutozidisha uzito inaanza kazi rasmi kesho baada ya kusitishwa kuendelea Januari Mosi, mwaka huu.
Kusitishwa kwa sheria hiyo kulitokana na kutofungwa kwa vifaa katika mizani na utoaji elimu kwa madereva na wamiliki.Kauli hiyo imekuja wakati wa utoaji wa elimu kwa madereva katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Mkuu wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Julias Chambo.
Alisema awali walisitisha sheria hiyo kuanza Januari Mosi kutokana na vifaa kutofungwa katika mizani na kwa muda wa miezi miwili walikuwa wanaendelea na utoaji wa elimu.Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Mkoa wa Songwe, Batista Nyengo, alisema barabara zimeharibiwa kutokana na baadhi ya watumishi wa usalama barabarani kusimamisha magari sehemu ambazo si rafiki.
Nao baadhi ya madereva walisema kuwa sheria hiyo wameipokea, lakini wameiomba Tanroads kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri kwa kusimamisha magari barabarani kwa kuwa baadhi ya maofisa wa usalama sio waadilifu kutokana na kusimamisha magari sehemu ambayo mtu hawezi kuegesha vizuri.
Anania Mjavile, dereva wa lori alisema matukio mengi ya ajali za barabarani yanatokana na barabara kuwa mbovu licha ya madereva kupewa lawama kuwa ni wazembe na kwamba endapo zitakarabatiwa na kuwekwa alama matukio ya ajali yatapungua.
0 comments:
Post a Comment