MKE
wa Rais Mama Janeth Magufuli amekabidhi chakula kwa ajili ya futari
wakati huu wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa vituo vinne vya
kulea watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu Jijini Dar
es salaam.
Vyakula
hivyo vimekabidhiwa leo tarehe 18 Juni, 2016 katika ofisi ya Mke wa
Rais Ikulu Jijini Dar es salaam vimejumuisha Mchele kilogramu 500,
Sukari kilogram 500 na Tende kilogramu 28.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi vyakula hivyo, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli
aliyeongozana na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewatakia heri
Waislamu wote katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwasihi
waendelee kuliombea Taifa amani na utulivu.
“Tunawatakia
mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, katika kipindi hiki
tunawaomba mzidi kuiombea nchi yetu amani, viongozi wetu wa nchi na
watanzania wote kwa ujumla, nchi ikiwa na amani ndio mambo mengi mazuri
yanaweza kufanyika”
Kwa
niaba ya vituo vilivyopatiwa vyakula hivyo, Mwenyekiti wa Kituo cha
Charambe Islamic Center Dkt. Haruni Kondo amemshukuru Mke wa Rais kwa
kutoa vyakula hivyo na ameeleza kuwa kitendo hicho kinaonesha mshikamano
na ushirikiano walionao watanzania wote bila kujali tofauti ya dini,
kabila wala maeneo wanayotoka.
“Kwa
hiyo ndugu zangu mna imani ya kikristo lakini mnatambua waislamu ni
ndugu zenu, wote tunajenga nyumba moja, mshikamano ndio tunu
tuliyoachiwa na Baba yetu wa Taifa, leo mmeguswa kuona wenzenu tunafanya
ibada na nyinyi mmeingia kwenye ibada, sasa ibada ya kutoa ni ibada
kubwa sana, sio nchi nyingi katika Afrika zinafanya kitendo hiki, watu
hawaelewi, ni nchi chache sana ambazo imani moja inaunga mkono imani
nyingine, lakini sisi waislamu tunalitambua hili hata toka kipindi
ambacho mtume wetu SWA anapigana kusimika dini hii kwa waumini alipata
nusura kwa wakristo”
Vituo vilivyokabidhiwa vyakula hivyo ni Charambe Islamic Center, Tasofe Lqadiria, Nur Twarigatu Lqadiria na Zawiyatul Lqadiria.
0 comments:
Post a Comment