Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei, 2016 umeongezeka kidogo hadi kufikia
asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.1 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2016.
Hii
inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka
ulioishia mwezi Mei, 2016 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi
iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2016.
Kwa
mujibu wa wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dkt. Albina Chuwa iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam, kuongezeka kwa
Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za
baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Baadhi
ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni
pamoja na mahindi kwa asilimia 1.5, unga wa muhogo kwa asilimia 6.2,
nyama ya kuku kwa asilimia 2.6, njegere kwa asilimia 5.8, mihogo mibichi
kwa asilimia 8.0 na ndizi za kupika kwa asilimia 2.7.
Bidhaa
zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja
na mafuta ya taa kwa asilimia 2.9, mkaa kwa asilimia 2.5, dizeli kwa
asilimia 4.6, petroli kwa asilimia 2.5 na vifaa vya michezo kwa asilimia
7.8.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 unaopimwa kwa
kipimo cha mwezi umebaki kuwa asilimia 0.5 kama ilivyokuwa mwezi Aprili,
2016. Aidha, Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 103.00 mwezi Mei, 2016
kutoka 102.46 mwezi Aprili, 2016.
Aidha,
ulinganifu wa Mfumuko wa Bei kwa baadhi ya nchi za Jumuia ya Afrika
Mashariki, taarifa hiyo inaonyesha kuwa Mfumuko wa Bei nchini Uganda kwa
mwezi Mei, 2016 umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia
5.1 kwa mwezi Aprili, 2016.
Kwa
upande wa Kenya, Mfumuko wa Bei umepungua hadi kufikia asilimia 5.00
kwa mwezi Mei, 2016 kutoka asilimia 5.27 iliyorekodiwa mwezi Aprili,
2016.
0 comments:
Post a Comment