Friday, 20 May 2016

Serikali Yajibu Hoja za Kivuko cha MV Dar es Salaam.

Serikali imejibu hoja za upinzani kuhusu uuzwaji wa nyumba za Serikali na kutetea ununuzi wa kivuko cha MV Dar es Salaam ambacho kilitakiwa kufanya safari zake kati ya Dar na Bagamoyo.

Hoja hizo ziliibuliwa katika hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, James Mbatia akitaka kutekelezwa kwa azimio la Bunge la urejeshwaji wa nyumba hizo serikalini lililotolewa Aprili 2008.

Pia, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha upungufu katika kivuko cha MV Dar es Salaam ambao ni kutolipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kutokuwa na kasi kadri ya mkataba na kutokuwapo hati ya makabidhiano.

Hoja hizo za upinzani zilijibiwa juzi jioni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alisema hakuna taratibu zozote zilizokiukwa wakati wa ununuzi wa kivuko hicho ambacho kwa zaidi ya mwaka hakijaanza kazi.

Alisema wizara ilipata taarifa ya CAG ambayo ilibainisha upungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na kivuko hicho kununuliwa kwa Dola za Marekani 4.9 milioni (Sh7.9 bilioni) bila kulipiwa VAT, lakini akasisitiza kwamba hakukuwa na ukiukwaji wowote wa taratibu za ununuzi.

“Ni kweli kivuko kina mapungufu ikiwamo kasi ndogo, lakini hakuna ukiukwaji wowote wa taratibu wakati wa ununuzi. Temesa ilitangaza zabuni na baada ya maombi kupitiwa, kampuni ya MS Jones Gram Hansen ilishinda zabuni hiyo kwa kuwa na bei nafuu,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema baada ya kivuko kuletwa nchini Desemba 2014, kilifanyiwa majaribio na kubainika kwamba hakikuwa na kasi ya kuridhisha. Alisema makubaliano yalikuwa ni kujenga kivuko chenye kasi ya nots20, lakini hicho kilikuwa na kasi ya nots 15.7.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ilimtaka mkandarasi kurekebisha kasoro hiyo kwa gharama zake na kuwa ameshawasilisha andiko juu ya namna atakavyoifanya kazi hiyo.

“Mpaka sasa mzabuni huyo hajalipwa asilimia 10 ya malipo yaliyokubaliwa mpaka pale atakapokamilisha kazi hiyo. Kwa hiyo, taratibu zote zilifanyika kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kuhusu nyumba, Profesa Mbarawa alisema Serikali iliidhinisha mpango huo Aprili 24, 2008 baada ya kupata ridhaa ya Bunge ilipopeleka suala hilo kujadiliwa.

“Suala la uuzwaji wa nyumba za Serikali, pia taratibu zilifuatwa. Serikali ilileta mpango huo bungeni na kupata ridhaa ya wabunge wote. Kwa hiyo, niwaambie tu wabunge kwamba suala hili lilipata baraka zao,” alisema waziri huyo.

Uuzwaji wa nyumba za Serikali na ununuzi wa kivuko cha Mv Dar es Salaam vilifanyika wakati Rais John Magufuli akiwa waziri wa ujenzi kwa nyakati tofauti.

Kambi ya upinzani imekuwa ikisisitiza kwamba kuna ukiukwaji wa sheria uliofanyika wakati wa uuzaji wa nyumba na ununuzi wa kivuko hicho. Hata hivyo, Serikali imeshikilia msimamo wake kwamba sheria zilifuatwa

0 comments:

Post a Comment