Saturday, 21 May 2016

MBEYA CITY KUIKABILI NDANDA, SOKOINE KESHO.


KIKOSI cha Mbeya City Fc  kesho jumapili kinashuka kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika mchezo wa kufungia msimu  wa 2015/16 wa ligi kuu ya soka Tanzania  bara dhidi ya wageni wao Ndanda Fc 'wana kuchele' kutoka mkoani Mtwara.

Meneja  wa kikosi cha City, Geoffrey Katepa  amesema kuwa  nyota wote 18 wametayarishwa kwa ajili ya kuwakilisha  timu yao na wako kwenye hali nzuri na tayari kabisa kusaka ushindi.

“Kama unavyoona  tumemaliza mazoezi  muda huu, yalikuwa ni mazoezi mepesi kuelekea  mchezo wa kesho kila mmoja yuko vizuri na ana ari kubwa, jambo muhimu kwetu ni kushinda mchezo huo ili tumalize ligi kwa heshima, hatuna wasiwasi wowote tuko salama kwenye msimamo wa ligi, kumaliza kwa ushindi kutatuweka kwenye mapumziko mazuri  kwa matayarisho ya msimu mpya”, amesema Katepa.

Kuhusu  majeruhi Katepa  alisema kuwa City itakosa huduma ya nahodha na mlinzi shupavu wa kushoto Hassan Mwasapili aliye majeruhi kufuatia maumivu ya nyama za paja  yanayomkabili, pia  Temi Felix na Deo Julius  hawatakuwa sehemu ya mchezo wa kesho kupisha majeraha waliyonayo.

“Mkuu wa kitengo  chetu cha utabibu Dr Joshua kaseko, amenieleza asubuhi kuwa  tutawakosa wachezaji hao kutokana na majereha waliyonayo hii ina maana kuwa wataonekana uwanjani  wakati wa matayarisho ya msimu mpya, mwalimu tayari kashafanya utaratibu wa wale wataochukua nafasi zao hivyo tuna uhakika wa kuingia uwanjani na kikosi kilicho bora licha ya kuwakosa hao tutahakikisha ushindi unapatikana.

0 comments:

Post a Comment