Wednesday, 18 May 2016

MAMLAKA ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) yatoa notisi kwa wapangaji wa nyumba 174 ambazo ni za ghorofa mbili kuhama.





MAMLAKA ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imetoa notisi kwa wapangaji wa nyumba zake 174 zilizopo Kikuyu Mjini hapa ambazo ni za ghorofa mbili kuhama ili kupisha ukarabati mkubwa wanaotaka kufanya.

Akizungumza jana Ofisa habari na mahusiano wa CDA, Angela Msimbila alisema, walishatoa notisi ya siku saba ya kuwataka wapangaji wote kuhama ili kupisha ukarabati mkubwa unaotakiwa kufanyika kwenye nyumba hizo ukiwemo wa majengo, mifumo yote ya umeme, vyoo na majitaka.

Amesema awali wapangaji hao walikuwa wakilipa kodi ya Sh. 18,000 kwa nyumba yenye vyumba viwili na sebule, kodi ya Sh 20,000 kwa nyumba yenye vyumba viwili, sebule na sehemu ya kulia chakula, kodi ya Sh 22,000 kwa nyumba ya vyumba vitatu, sebule na sehemu ya kulia chakula.

Hata hivyo mwaka 2008 mamlaka hiyo ilifanya mabadiliko ya kodi  za nyumba katika maeneo mbalimbali ikiwepo nyumba za Maghorofa ya Kikuyu, mabadiliko hayo yaliongeza viwango vya kodi katika nyumba hizo kwa kuzingatia uwiano wa kodi katika soko.

Amesema ongezeko hilo la kodi lilitaka wapangaji kulipa kodi kati ya Sh. 50,000, Sh,55,000 na Sh. 65,000 jambo ambalo hawakukubaliana nalo na kwenda kufungua kesi mahakamani

“Baada ya ukarabati kodi katika nyumba hizo zitapanda  na kuwa Sh, 120,000, Sh130,000 na Sh l50,000 na wapangaji watakaokuwa na vigezo watapangishwa nyumba hizo na mamlaka” alisema
Msambira alisema mwaka 2008 wapangaji walipeleka kesi mahakamani (Baraza la Ardhi) kupinga kupandishwa kwa viwango vya kodi na kesi hiyo ikaanza kusikilizwa.

Amesema tangu kipindi hicho kumekuwa na mwendelezo wa kesi mbalimbali za kupinga ongezeko la kodi mpaka mwaka 2016.
Alisema kutokana na kesi hizo wapangaji  zaidi ya 150 waligoma kulipa kodi tangu wakati huo na kuisababishia mamlaka hasara kubwa.
Msimbila alisema CDA imekuwa ikikusanya kodi jumla ya Sh. Milioni 3.4 kwa mwezi  bila kodi ya ongezeko la Thamani(VAT) na ukitoa kodi hiyo mamlaka imekuwa ikipata Sh. Milioni 2.9.


Alisema mamlaka hiyop imetenga fedha za ukarabati wa majengo hayo katika mwaka wa fedha 2015/2016, ilitangaza zabuni na kumpata mkandarasi wa kufanya ukarabati.
Alisema  kwa sasa mamlaka hiyo imejipanga kufanya zoezi la kuwaondosha wapangaji watakaokaidi ilani ya kuwataka kutoka ndani ya siku saba kwa kutumia dalali.

0 comments:

Post a Comment