Sunday, 10 March 2019

Wananchi wilayani Mbogwe watahadharishwa juu ya njaa.

Wananchi wilayani Mbogwe watahadharishwa juu ya njaa.

Wananchi Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita imewatahadharisha wananchi wake kutumia kwa umakini akiba ya chakula waliyonayo ili kukabiliana na tishio la njaa linaloinyemelea halmashauri hiyo.

Tahadhari hiyo imetolewa jana Machi 9, 2019 na Kaimu Mkurugenzi, Samuel Makala alipokuwa akielezea hali hiyo ambayo imesababishwa na mabadiliko ya tabianchi yaliyochangia ukame uliokausha mbegu zilizopandwa msimu wa kilimo.

"Tuna hofu sana na mwaka huu kwani mvua hazijanyesha kabisa hivyo wakulima hawakuweza kupanda. Tunawaasa watumie chakula vizuri na walime mihogo na viazi lishe mazao yenye uvumilivu na ukame", amesema Makala.

Makala amekiri baadhi ya maeneo hasa kijiji cha Bwelwa ambacho wakazi wake wanategemea mpunga na pamba kama mazao la biashara na mahindi kwa ajili ya chakula kwa misimu mitatu hawakupata mazao kutokana na ukame.

Katika kuwanusuru wanakijiji hao 12,431 wa Bwelwa, meneja mawasiliano wa Oxfam, Kisuma Mapunda amesema shirika hilo likishirikiana na wadau wengine wamewapatia mbinu mbadala za kujikwamua kiuchumi wananchi ikiwa ni pamoja na ufugaji wa samaki, nyuki, utengenezaji batiki na kilimo cha viazi lishe.

Mmoja wa wakulima Leticia Elia, amesema hali ya chakula katika eneo hilo ni mbaya kwa mwaka huu kutokana changamoto hiyo.

“Mwaka huu tunaona kabisa kutakuwa na upungufu mkubwa, hata waliopanda mahindi nayo hayajazaa. Wananchi wa hapa tuna hali ngumu tatizo ni ukosefu wa mvua," amesema Elia.

Hata hivyo, Elia amewashukuru watu wa Oxfam waliofika kijijini hapo mwaka 2017 na kuwashauri wakazi kujiunga kwenye vikundi ili waweze kuwasaidia.

Amesema tayai wamejiunga kwenye kikundi cha kina mama 17 wanaojishughulisha na kilimo cha viazi lishe na ulimaji wa mboga mboga.

"Tutaendelea na kilimo, ila kama kina mama lazima tubuni miradi ya kutuingizia kipato. Tukitegemea mvua watoto hawatakwenda shule na mahitaji mengine tutakosa,’’ amesema Elia.

Naye Emmanuel Bwire amesema wamejiunga katika kikundi cha watu watano wanajihusisha na ufugaji nyuki na samaki wakati wakisubiri kuona kama mvua zitanyesha ili kuotesha mbegu za mpunga.

0 comments:

Post a Comment