Monday, 11 March 2019

Usajili Brela sasa kidigitali

Usajili Brela sasa kidigitali


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), umeanzisha mfumo mpya wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) kwa lengo la kuboresha zaidi huduma kwa wateja wake.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Emanuel Kakwezi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema kuanzia sasa, huduma zote zitatolewa kwa njia ya mtandao.

Alisema tayari wameshaanza kutoa elimu kwa wadau wao ambao ni wafanyabiashara, wasomi na wananchi wote ili kuanza kufanyia kazi mabadiliko hayo.

Kakwezi alisema mabadiliko hayo yamekuja baada ya kuona wateja wengi wamekuwa wakishindwa kujaza fomu za awali ambazo zilikuwa za karatasi.

Alisema ujazaji wa fomu za awali ulikuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kupishana kwa taarifa na kusababisha kila wakati taarifa kurudishwa au kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara.

"Wakati mwingine watu walikuwa wanaturudishia fomu zikiwa hazina vigezo vinavyotakiwa au hazijakamilika kabisa, na ndiyo maana wakati mwingine maombi mengi ya wateja hukataliwa kwa sababu ya kutofuata vigezo vinavyotakiwa," Kakwezi alisema.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni wateja kutofuatilia maelekezo yanayotakiwa ili kukizi vigezo na kutofuatilia maelekezo yaliyoko katika fomu husika, hivyo kusababisha usumbufu wa kurudia mara nyingi kujaza fomu hizo.

0 comments:

Post a Comment