Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji mkoani Lindi linaloandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Machi 26 mwaka huu.
Aidha Samia atazindua kiwanda cha kusaga unga wa mhogo ambapo ni sehemu ya uwekezaji katika mkoa huo katika ziara yake itakayoanza Machi 22 hadi 28, mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema hayo katika mahojiano yaliyofanywa na Shirika la Habari la Utangazaji (TBC) yakimhusisha pia Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah, yaliyozungumzia Jukwaa hilo na Fursa za Biashara na Uwekezaji.
Zambi alisema fursa za biashara na uwekezaji zipo tele katika mkoa huo, ambazo hazijatumika kikamilifu zikiwemo za viwanda, utalii, kilimo, madini, utalii na nyinginezo.
Amesema wanaishukuru TSN kwa kuandaa jukwaa hilo, kwani kwao ni kama hatua ya kuupeleka mkoa mbele zaidi. Aliwakaribisha wawekezaji kwenda kuwekeza mkoani Lindi, kwa kuwa hivi sasa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam imeshajaa.
Amesema hivi sasa mkoa umetoa kipaumbele katika ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho, ufuta na mihogo, kwani ni mazao yanayolimwa kwa wingi. Kwa upande wake, Tuma alisema jukwaa hilo ni fursa adhimu kwa wananchi, kuweza kushiriki na kuangalia fursa wanazoweza kuzitumia.
Tuma alisema wananchi wote wanakaribishwa katika jukwaa hilo, kwa kuwa ni sehemu ambayo watakutana na mamlaka za nchi ili waweze kueleza changamoto zinazowakabili, pia kuona namna gani wanaweza kutoka hapo walipo na kufikia maendeleo.
0 comments:
Post a Comment