Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umesema uamuzi wa kumpokea Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, umefuata taratibu sawa na wanachama wengine lakini pia umetoa somo kwa vijana kufahamu hakuna mkamilifu kwenye safari ya kisiasa.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James, kama Lowassa angepokelewa kinyume na chama hicho, umoja huo ungesimama kukemea.
“Tunawapongeza viongozi wakuu wa Chama kwa kitendo cha kumpokea Lowassa. Amerudi CCM kwa kuzingatia taratibu zote kama wanachama wengine. Lowassa ni raia wa Tanzania kuhamia Chadema hakumuondolea haki ya kurejea CCM,” amesisitiza
Hata Bw.James amesema kuwa milango ipo wazi kwa wanasiasa wengine wenye kutaka kuhamia CCM kwani mtaji wa chama chochote cha siasa ni wanachama.
Aidha Bw. James alikemea vitendo vya baadhi ya wanasiasa kutumia lugha zisizokuwa na staha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli, akisema kitendo hicho hakikubaliki.
“Vibaraka hao wasidhani habari mbaya wanazopeleka nje ya nchi, mazuri yanayofanyika hayafahamiki. Wamejipa kazi ya kupotosha kwa lengo la kuikomoa serikali lakini wafahamu wanaowaumiza ni wananchi.
“Niwaambie, wataiona faida ya Rais Dk. Magufuli, baada ya kumaliza muda wake. Ni katika utawala wake ambapo mtu anapata ajira bila kuulizwa kabila lake, wananchi wanahudumiwa ipasavyo na wafanyabiashara wanapata zabuni bila upendeleo,” amesema James
Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na viongozi waandamizi wa UVCCM, alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa watiifu kwa sheria za nchi.







0 comments:
Post a Comment