Monday, 11 March 2019

Ilemela itazidi kupaa Kitaaluma - Afisa elimu Mwanza

Ilemela itazidi kupaa Kitaaluma - Afisa elimu Mwanza


Kitendo cha kuwakutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka shule za binafsi na za serikali kwa kuwapongeza na kuwapa zawadi kutokana na kupata matokeo mazuri ya mtihani wa darasa la saba na kidato cha nne kwa miaka mitatu mfululizo kilichofanywa na halmashauri ya manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Angeline Mabula hakijawahi kutokea nchini na kamwe hakitatokea na kikitokea itakuwa wamejifunza kwa Ilemela.

Kauli hiyo imetolewa leo na mgeni rasmi katika sherehe za kuwapongeza walimu hao ambae ni afisa elimu mkoa wa Mwanza Mwalimu Michael Ligola wakati akizungumza na walimu hao huku akimpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa kuanzisha utaratibu huo sanjari na madiwani wa manispaa hiyo kwa kutokuwa na migogoro na walimu wa shule za kata zao.

"Nakiri kusema haijapata kutokea na huenda isitokee na wengine wowote watakaofanya watasema tunaiga kwa Ilemela," alisema.

Aidha mgeni huyo ameahidi kushirikiana na uongozi wa manispaa ya Ilemela katika kuhakikisha halmashauri hiyo inazidi kufanya vizuri katika sekta ya elimu sambamba na kutatua changamoto za elimu.

Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt Angeline Mabula amewashukuru wadau anaoshirikiana nao kupitia taasisi yake ya The Angeline Foundation inayosaidia kwa kiasi kikubwa uimarishaji wa miundombinu muhimu ya shule ikiwemo madarasa, ofisi na vyoo huku akiwahakikishia kutimiza ahadi yake ya kuwapatia viwanja zaidi ya 1600 walimu wa manispaa hiyo kwa gharama nafuu ya shilingi milioni moja na nusu itakayolipwa kwa miezi kumi kwa kiwanja cha ukubwa  wa pembe mraba 500 mpaka 700.

Nae Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Taifa, Mwalimu Christopher Banda ambae baada ya kufurahishwa na jitihada zilizofanywa na Mhe Dkt Angeline Mabula katika kuimarisha sekta ya elimu ndani ya jimbo lake akaamua kuahidi kuleta mradi mkubwa wa kuwajengea uwezo walimu mkoani Mwanza ili ikawe chachu katika kuongeza zaidi jitihada za kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa

Sherehe ilihudhuriwa na madiwani wote wa manispaa ya Ilemela, viongozi wa chama cha walimu mkoa na wilaya ya Ilemela, maafisa elimu kutoka halmashauri ya jiji la Mwanza na halmashauri jirani, viongozi wa vyama vya siasa, mkuu wa wilaya ya Ilemela, mkurugenzi, na wakuu wake wote wa idara za manispaa hiyo huku zawadi ya mshindi wa kwanza kitaaluma kwa elimu msingi ikichukuliwa na shule ya msingi Bwiru, ya pili Gedeli na ya tatu Kitangiri wakati kwa elimu sekondari nafasi ya kwanza ikienda kwa shule ya Bwiru wavulana, ya pili Mwinuko na tatu Nyamanoro.

Kwa shule binafsi msingi nafasi ya kwanza ilichukuliwa na shule ya Nyamuge, ya pili Lojoma na tatu Ilemela huku elimu sekondari nafasi ya kwanza ikienda kwa Morning star, ya pili Loreto na tatu Maris.

0 comments:

Post a Comment