Hospitali za mikoa zatakiwa kuongeza ubunifu
Matumizi ya fedha za ndani katika Hospitali za umma zinaweza kutumika katika kutatua uhaba wa watumishi katika ngazi zote na kuacha tabia ya kuisubiri Serikali kufanya kila kitu.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ambae pia ni Mbunge wa Biharamulo, Oscar Mukasa wakati kamati hiyo ilipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika kujionea hali ya utoaji huduma za afya.
"Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ni moja ya maeneo ambayo nimewahi kushuhudia matumizi bora ya fedha za ndani katika kutatua ikama ya watumishi hata ngazi ya Madaktari na Wauguzi," amesema.
Akijibu hoja za baadhi ya Wabunge Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha vituo vya Afya na kujenga Hospitali za Wilaya ili kupunguza msongamano katika Hospitali za Rufaa za mikoa.
"Serikali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine tumeamua kuboresha vituo vya Afya ili kupunguza mzigo mkubwa kwa Hospitali za Rufaa, na katika Wilaya ya Kinondoni kuna vituo vya afya viwili vinavyojengwa" alisema Dkt Ndugulile
Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa Serikali inatambua kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaoenda kupata huduma za Afya ni watu wa misamaha, hivyo kupoteza zaidi ya Bilioni mbili kwa mwezi na hiyo ni kutoka Julai 2018 mpaka mwezi Februari 2019, hali inayorudisha nyuma shughuli za utoaji huduma bora za Afya.







0 comments:
Post a Comment