Serikali ya Kenya
imeanza kutekeleza sheria mpya kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, kama
njia ya kutoa ajira zaidi kwa Wakenya na kudhibiti ongezeko la waajiriwa
kutoka nchi za nje.
Serikali ya Kenya imesema kuwa, wafanyikazi
wa mashirika ya kimataifa kutoka ughaibuni wamekuwa wakipokea malipo na
marupurupu bora kuliko wakenya licha ya kufanya kazi sawa.Taifa hilo, kupitia bodi ya usimamizi wa mashirika hayo, imetangaza kuwa mashirika hayataruhusiwa kuwaajiri raia wa nchi za nje kwa nafasi za kazi zinazoweza kutekelezwa na Wakenya.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo, Fazul Mohamed, masharti hayo yamekuja baada ya serikali kutathmini jinsi mashirika hayo yalivyokuwa yakifanya kazi.
'Tumechunguza na kupata kuwa hakuna usawa katika malipo na mipango mingine yanayotolewa kwa ajili ya kazi. Waajiriwa wa nchi za kigeni wanalipwa mara nne bora kuliko wakenya na hiyo sio sawa,'' alisema Fazul.
Hatua hiyo imesifiwa na wakenya kwenye mitandao ya kijamii. Wengi, wakiwemo waliowahi kufanya kazi katika mashirika hayo, walionekana kuunga mkono hatua hiyo.
Taifa la Kenya limekuwa likijitahidi kuzuia ongezeko la idadi ya vijana wasiokuwa na ajira na hatua hii inaonekana kama njia ya kukabiliana na uhaba wa ajira.
''Tunahisi kuwa Wakenya waliofuzu kufanya kazi za mashirika, hawapewi nafasi hizo licha ya kupokea elimu inawafanya kuwa na uwezo wa kazi hizo, mikakati hizi zitaleta nidhamu katika sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali na kuwapa motisha wahudumu wa kenya wanaofanya kazi katika mashirika hayo,'' aliongeza Fazul.
Hata hivyo, baadhi ya wakuu wa asasi zisizo za kiserikali, wametofautiana na agizo la serikali ya Kenya. ''Ni ukweli malipo ya wafanyikazi wa kigeni ni makubwa, lakini kila muajiriwa hufanya kazi kulingana na mkataba wa kazi'' alidai Mkurugenzi wa shirika moja la kimataifa nchini Kenya.
Msimamizi huyo, amefafanua kuwa tofauti za mishahara na marupurupu kati ya waajiriwa wa Kenya na raia wa nchi za nje zimetokana na changamoto za kufanya kazi kwa raia hao nchini Kenya. ''Wengi wao wametengana na familia kuja kufanya kazi mbali na taifa lao. Hali ni tofauti na raia wa Kenya ambaye yupo nyumbani,''.
Bodi ya mashirika hayo imeahidi kuyachukulia hatua mashirika yatakayokiuka masharti hayoi ikiwemo kuwanyima vibali wahudumu wa mashirika hayo na hata kuyapokonya mashirika hayo usajili wao hapa Kenya.
''Tutakaguzi stakabadhi za wale wahudumu kutoka nchi za nje na iwapo tutaona kuwa kazi hiyo inaweza kutekelezwa na Mkenya, basi hatutapitisha wapewe vibali, na mashirika yatakokosa kutimiza sheria hizi, basi tutayapokonya usajili wao, alimaliza Fazul''.
0 comments:
Post a Comment