Friday, 3 June 2016

Jinamizi la Escrow laibuka tena, Tibaijuka awatajataja wahusika.

Jinamizi la kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow bado linamsumbua mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka baada ya kuliibua kwenye semina ya mapambano dhidi ya ufisadi, akichongea wabunge ambao hawajaguswa.

Profesa Tibaijuka alipoteza uwaziri wa nyumba, ardhi na makazi kwenye sakata hilo baada ya kubainika kuwa aliingiziwa fedha zinazoonekana zilitoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja na Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Profesa Tibaijuka alikuwa mmoja kati ya viongozi wa ngazi ya waziri, mbunge, jaji na viongozi wa dini walioingiziwa fedha ambazo zinatokana na Sh306 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti hiyo.

Akichangia katika semina hiyo inayolenga kuwajengea wabunge uwezo wa kupambana na ufisadi na ambayo iliandaliwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Ufisadi (ACFE), Profesa Tibaijuka alisema wakazi wa jimbo lake walimchagua kwa mara nyingine licha ya tuhuma za Escrow kwa sababu hawakuziamini.

Alisema fedha hizo za Escrow zilitoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kwenda benki ya Stanbic na Mkombozi, lakini cha ajabu majina ya watu waliopewa fedha kupitia benki moja yalitolewa na yale ya benki nyingine yalifichwa.

Alisema inakuwaje yeye anakuwa katika tuhuma, wakati aliyempa fedha hizo hatuhumiwi.

Watu waliotajwa kwenye sakata hilo ni wale waliopewa fedha zilizopitia benki ya Mkombozi, lakini hadi sasa wale waliopewa fedha zinazodaiwa kuwa ni taslimu kutoka Stanbic hawajatajwa.

Alisema sheria pekee yake haiwezi kufanya lolote katika mapambano dhidi ya ufisadi na hakubaliani na wabunge wanaosema kuwa hata kama mahakama imeshindwa kuthibitisha ufisadi, watuhumiwa wataifishwe mali zao.

“Sisi wabunge hatukuja kufanya kazi hiyo, tumekuja kutunga sheria ili zisaidie katika kutuongoza,” alisema.

“Ni vyema kuzungumzia unyofu wa watu kwa kuanzia katika shule, makanisa, misikiti na wabunge.”

Aliituhumu Takukuru kuwa inakubali kutumiwa kwa kuchagua kesi za kuchunguza.“Tume ya Maadili ndio usiseme,” alisema.

“Mie nimeshawahi kushtakiwa Tume ya Maadili, najua kuwa kuna mbunge mwenzetu hapa alipata fedha za Escrow, lakini kwa sababu hakuwa mzungumzaji ameondoka bungeni wala hakuna mtu anajua kama alipata. Unaona jinsi ambavyo hawa watu hawako makini,” alisema.

Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu alilia na watu aliowaita wazushi kwamba wanawazushia wenzao kuchukua rushwa wakati hakuna ukweli.

0 comments:

Post a Comment