Mabingwa Tanzania Bara, Yanga wamejihakikishia kupata Dola 150,000 (Sh 330 milioni), baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Sagrada Esperanca kwa jumla ya mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Sagrada Esperanca, Dundo baada ya jana kufungwa bao 1-0 hivyo kusonga mbele kutokana na ushindi wa mabao 2-0 iliopata Dar es Salaam.
Kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alibuka shujaa kwa kuokoa penalti katika dakika 85, na kuihakikishia Yanga kusonga mbele katika mashindano hayo.
Penalti hiyo ilitolewa katika dakika ya 82 na kusababisha mechi kusimama kwa dakika tano baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kupewa kadi nyekundu na wachezaji wa Yanga kumsonga mwamuzi kwa madai ya kuonewa.
Maofisa wa usalama wa Angola walilazimika kuingia uwanjani na kumtoa mwamuzi huku wakiwasihi wachezaji wa Yanga watulie na kuendelea na mchezo.
Baada ya hali ya hewa kutulia na mchezo kuendelea, penalti hiyo ilipigwa na Dida aliicheza jambo lililoamsha ari kwa wachezaji wa Yanga na kuwachanganya wapinzani wao.
Kutokana na kadi hiyo, Yanga ililazimika kumtoa Amissi Tambwe na kumwingiza Kelvin Yondani katika dakika za lala salama ili kulinda lango lake.
Bao pekee la wenyewji lilipatikana katika dakika ya 25 mfungaji akiwa Love Kabungula.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), timu nane zinazofuzu hatua ya makundi zinajihakikishia kuondoka na Dola 150,000 (Sh 330 Milioni) kwani timu itakayoshika mkia katika michuano hiyo itakayochezwa kwa mtindo wa ligi, itapata kiasi hicho cha fedha.
Timu zitakazoshika nafasi ya pili na tatu katika moja ya makundi mawili yatakayopangwa kwenye ligi hiyo, zitaondoka na kitita cha Dola 239,000 (Sh525 milioni). Bingwa wa mashindano hayo atavuna Dola 625,000 (Sh1.3 bilioni) wakati mshindi wa pili atapata Dola 432,00 (Sh950 milioni).
Katika mchezo huo, Waangola walionyesha dhamira ya kupata mabao ya mapema kwani katika dakika ya 10 tu ya mchezo walifanya shambulizi kubwa langoni mwa Yanga lakini mabeki wa Yanga walikuwa imara. Walishambulia tena bila mafanikio katika dakika ya 25.
Yanga ilijibu mapigo katika dakika za 14, na 33 kupitia kwa Tambwe, Donald Ngoma na Mbuyu Twite lakini jitihada zao hazikuzaa matunda.
Kutokana na presha ya mchezo huo, wachezaji wa Yanga, Thaaban Kamusoko, Tambwe, Cannavaro, Vincent Bossou na Dida walionyeshwa kadi za njano.
Katika kipindi cha pili, Yanga ilifanya mabadiliko katika dakika ya 60 kwa kumtoa Kamusoko na kumwingiza Deus Kaseke.
Vurugu uwanjani;Baada ya mchezo huo, wachezaji na viongozi wa Yanga walilazimika kubaki ndani ya vyumba vya kubalishia nguo kutokana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na mashabiki wa Esperanca.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema katika ghasia hizo, alipoteza saa yake ya mkononi huku akilalamikia kitendo cha baadhi ya maofisa usalama kutaka kumpora simu yake ya mkononi.
Mchezo mwingine, Etoile du Sahel nayo ilisonga mbele katika michuano hiyo licha ya kufungwa bao 1-0 na Mounana ya Morocco. Katika mchezo wa kwanza, Sahel ilishinda 2-0.
Kikosi.Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Simon Msuva.
Akiba.Ali Mustafa, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Salum Telela, Mateo Anthony, Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya







0 comments:
Post a Comment