WAZIRI
Mkuu, Kasim Majaliwa, ametoa onyo kwa wafanyabiashara wanaodhulumu
wakulima kwa kununua mazao kwa kuyafunga kwenye magunia bila kuzingatia
vipimo sahihi maarufu kama lumbesa, na kutaka viongozi kuanzia ngazi ya
vijiji mpaka mikoa kusimamia.
Alisema
serikali itapambana na wafanyabiashara wanaoendelea kulazimisha
kufungasha mazao katika magunia bila kuzingatia vipimo sahihi hivyo
kuwapunja na kuikosesha serikali mapato.
Akijibu
swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Saumu Sakala (CUF) katika
kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Majaliwa alikiri
kuwa serikali ilishazuia matumizi ya kipimo cha lumbesa na kuahidi
kwamba awamu hii, itakomesha dhuluma hiyo.
Awali
mbunge huyo alitaka kauli ya serikali dhidi ya vitendo hivyo kuendelea
ingawa kupitia viongozi mbalimbali wa serikali, vilishapigwa marufuku.
Waziri
Mkuu alitoa mwito tena kwa wakuu wa wilaya, halmashauri zao, maofisa
biashara katika halmashauri hizo kuhakikisha unyonyaji huo unakomeshwa.
Pia
aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata, kuhakikisha wafanyabiashara
wadogo wanaouza mazao kwenye maeneo yao, hawauzi mazao kwa kipimo cha
lumbesa.
Katika
hatua nyingine, Majaliwa alisema tayari maelekezo yametolewa kwa Wakala
wa Vipimo, kuhakikisha biashara yote ya mazao ya kilimo nchini yanauzwa
kwa vipimo vya kilogramu na siyo kwa kufungashwa lumbesa.
0 comments:
Post a Comment