Friday, 20 May 2016

MKAPA KUONGOZA TIMU YA USULUHISHI WA MGOGORO WA BURUNDI.


Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ameteuliwa kuongoza mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi ikiwa ni jitihada za viongozi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki katika kuleta amani ya kudumu nchini humo.

Mheshimiwa Mkapa, aliyeteuliwa na Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki atakuwa kiongozi wa timu ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi katika kikao kitakachofanyika kuanzia mei 21 hadi 24 mwaka huu, katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa ulipo jijini Arusha (AICC), ambapo inatazamiwa wadau wa pande zote za mgogoro watashiriki.

Aidha, Mkutano huo wa 17 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ulifafanua kuwa Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Museveni, ataendelea kuwa msuluhishi wa kudumu kutoka jumuiya hiyo.

Serikali ya Burundi ilikubali kufanyika usuluhishi na iko tayari kushiriki katika mazungumzo ya amani yanayofanywa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yakihusisha wadau wote wa siasa nchini Burundi ikiwa ni jitihada za kuumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.(P.T)

0 comments:

Post a Comment