Beatrice Ndomba akiwa amekatwa miguu.
RUVUMA: Beatrice Ndomba (23)
amelazimika kukatisha masomo kwenye Chuo cha Uhasibu jijini Mbeya mwaka
2012 baada ya kuugua ugonjwa uliogharimu miguu yake.
Msichana huyo anasema kuwa,
mwaka 2012 akiwa chuoni hapo, alianza kujisikia hali ya homa, ikabidi
arudi kwao, Songea mkoani Ruvuma kwa matibabu.
Alisema tatizo lilianza mwaka 2012 akiwa
amejiunga na masomo ya stashada ya uhasibu kwenye Chuo cha Uhasibu
jijini Mbeya ambapo alianza kupata maumivu makali kwenye mguu mmoja hali
iliyomsababishia kushindwa kuendelea na masomo.
Ilianza dalili ya homa kama malaria,
nilipewa dawa za SP ambazo hazikunisaidia, ndipo nilipelekwa Hospitali
ya Songea ambako nilitundikiwa dripu ya kwinini, pia haikusaidia, sasa
ikawa maumivu makali kwenye miguu yote.
Kabla ya kukatwa miguu
“Ilibidi nipelekwe Hospitali ya Rufaa ya
Misheni Peramiho ambapo madaktari walijitahidi lakini wapi. Miguu
ikaanza kuvimba na kuwa na rangi nyeusi, madaktari walishauriana na
kuamua kuichubua ngozi na kutibu vidonda.
“Uchunguzi zaidi ulifanywa na ulibaini
kuwa, mguu mmoja uliharibika hivyo waliamua kuukatia jirani ya goti,
ndipo ulemavu ukaanzia hapo.
“Madaktari waliniambia chanzo cha tatizo
ni matumizi ya dawa za SP na dripu la kwinini. Kidonda kiliendelea
kunisumbua kuanzia mwaka 2012 hadi 2014 na kunisababishia gharama kubwa
ya nauli na matibabu ya kwenda Peramiho kila baada ya siku moja.
“Wataalam wa viungo kwa walemavu wa
Wilaya ya Mbinga (Ruvuma) walitaka kunitengenezea mguu wa bandia,
lakini nilipochunguzwa kwa makini walibaini kunitengenezea mguu wa
bandia isingesaidia kwa kuwa mguu mwingine nao ulikuwa na matatizo
makubwa ambayo yalitakiwa kwanza kufanyiwa uchunguzi katika hospitali
nyingine.
“Julai 2014, Sista Lucy wa mjini Songea
alinisaidia nauli na fedha za matibabu na matumizi kwenda Hospitali ya
Misheni ya Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe ambayo inatajwa kuwa na
madaktari bingwa wa matatizo ya viungo vya binadamu ambako nilikatwa
mguu wa pili.
“Kwa sasa ndoto zangu za kuwa mhasibu
zimeyeyuka kwa kwa ulemavu huu, siwezi tena kuwa mhasibu badala yake
sasa napenda kujifunza zaidi lugha ya Kiingereza, kusomea kompyuta na
kujifunza ufundi wa kushona nguo na kudalizi vitambaa.
“Ndoto zangu sasa ni kufungua kiwanda
cha ushonaji kwa kuanzia nikipata mashine mbili nitaweza kujitegemea.
Nawaomba Watanzania wanisaidie mashine na misaada mingine, nitashukuru
sana,” alisema.
Beatrice ambaye ni yatima, ndiye mtoto
wa kwanza katika familia ya watoto tisa, anahitaji msaada wa hali na
mali katika kipindi hiki ambacho hana ajira zaidi ya kutegemea misaada
ya wahisani.
Hata hivyo, yeye na wadogo zake wamefadhiliwa kuishi kwenye nyumba moja iliyopo Ruhuwiko Manispaa ya Songea.
0 comments:
Post a Comment