Jumla ya asasi za kiraia (AZAKI) 16 zilizopo nchini zimetajwa kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 236 kwenye uchumi wa nchi ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 hadi 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya twaweza Aidan Eyakuze ameyasema hayo hii leo Novemba 5, 2019 jijini Dodoma mara baada ya kuwasilisha mada katika mkutano wa kwanza wa majadiliano wa wiki ya AZAKI ulioambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali za washiriki.
Amesema katika kipindi hicho cha miaka mitatu kuanzia 2016/18 mbali na kiasi hicho cha fedha kuchangia uchumi wa nchi pia jumla ya shilingi bilioni 19 zimelipwa na AZAKI kwa serikali kama makato mbalimbali ya kodi.
"AZAKI imekuwa ikichangia uchumi wa nchi na katika kipindi cha miaka mitatu mpaka kufikia mwaka 2018 ni shilingi bilioni 236 zimetumika ambapo pia katika upande wa kodi zimelipwa shilingi bilioni 19 kwa serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," amefafanua Eyakuze.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kiasi hicho cha kodi kilichokusanywa kinaweza kulinganishwa na makusanyo yaliyofanya na mamlaka ya mapato nchini (TRA) kwenye maji ya kunywa, vinywaji laini na sigara kwa mwaka 2018/19 ambayo yalikuwa ni shilingi bilioni 18.8.
“kodi hii iliyolipwa na AZAKI kwa serikali unaweza kuilinganisha kabisa na kodi iliyokusanywa na TRA mwaka 2018/19 katika mikoa ya Rukwa, Lindi, Simiyu, Songwe na Katavi kwa pamoja nadhanj.uanweza ona ni kiasi gani AZAKI ina mchango kwa Taifa ," Ameongeza Eyakuze.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society Francis Kiwanga amesema katika wiki hii ya AZAKI mbali na mambo mengine pia wanatarajia kuwa na kongamano linalojumuisha wadau mbalimbali ikiwemo serikali.
Amesema wakiwa katika mikutano ya ndani wanatarajia kujadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano na kuweka mikakati mbalimbali ili mchango wa asasi za kiraia uweze kutambulika na serikali.
Awali Mratibu wa asasi za kiraia nchini kutoka ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Denis Londo amezitaka taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika wiki hiyo kuzingatia yale yote watakayoyaazimia kwa maendeleo yao na nchi kiujumla.